Tuesday, May 17, 2011
MKUU WA SHIRIKA LA FEDHA DUNIANI IMF BW STRAUSS KUPANDA KUZIMBANI LEO JIJINI NEW YORK KUJIBU MASHTAKA IYANAYOMKABILI YA JARIBIO LA KUMBAKA MHUDUMU WA HOTEL JIJINI NHUMO.
Tukio hili limekuja wakati Strauss-Kahn akiongoza kampeni ya shirika lake kuyasaidia mataifa yanayotumia sarafu ya Euro kujikwamua kifedha na wiki chache tu kabla hajatangaza azma ya kuwania urais wa Ufaransa katika uchaguzi ujao.
Akiwa amefungwa pingu na akisindikizwa na maafisa wawili wa idara ya upelelezi ya New York, Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, Dominique Strauss-Kahn alionekana na uso wenye fadhaa usiku wa jana, ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana tangu shutuma za ubakaji dhidi yake zitajwe.
Wakili wake, William Taylor, amesema kwamba mteja wake alikubali kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu kwa hiyari yake, na kwamba atayakana mashitaka yote mahakamani hivi leo. Strauss-Kahn anashitakiwa kwa makosa matatu: jaribio la kubaka, shambulio la aibu na kumfungia mtu ndani bila ya ridhaa yake. Kama atatiwa hatiani, mashitaka haya yanaweza kumpeleka jela kwa kipindi kisichopungua miaka 15.
Minong'ono imeanza kuzagaa kwamba kesi hii dhidi ya Meneja Mkurugenzi huyo wa IMF ni mtego wa kisiasa kutoka ndani ya taasisi yake ya IMF na pia kutoka kwa washindani wake nchini Ufaransa, ambako anaonekana kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kushindana na rais wa sasa, Nicolas Sarkozy, kwenye uchaguzi wa mwakani.
Lakini polisi jijini New York inasema hakuna siasa yoyote, bali ni suala la kawaida la kisheria. Mapema polisi hiyo ilisema kwamba, mhudumu huyo wa kike alimtaja Strauss-Kahn kuwa ndiye aliyetaka kumbaka kwenye chumba chake kwenye hoteli ya Sofitel, wakati alipooneshwa kumtambua miongoni mwa wanaume wengine watano. Vyombo vya habari vya Marekani vimemnukuu mwanamke huyo akisema kwamba, aliingia chumbani kwa Strauss-Kahn, akidhani hamukuwa na mtu.
Nchini Ufaransa, ambako nyota ya kisiasa ya Strauss-Kahn ndiyo imeanza kung'ara, kumekuwa na wasiwasi kwamba huu ndio mwanzo wa mwisho wake. Dominique Paille wa chama kinachofuata siasa kali za mrengo wa kati, amesema kwa taifa la Ufaransa, hili ni tukio litakalochukuwa muda kusahaulika.
Hata hivyo, serikali ya Rais Sarkozy imeonya kwamba bado ni mapema mno kumuhukumu Strauss-Kahn, licha ya kwamba kesi hii sasa inaipa serikali hiyo fursa nzuri zaidi kwenye uchaguzi wa mwakani.
Naye kiongozi wa chama cha National Front, Marine Le Pen, anayependa kujijenga kama mwanamke anayepambana na dunia ya wanaume kwenye siasa, amesema kwamba kashfa hii haimshangazi sana. Katika kura za maoni za siku za karibuni Le Pen, amekuwa nyuma ya Strauss-Kahn kwenye nafasi ya uraisi.